Jumatano 22 Julai 2026 - 12:10
Maadhimisho ya Miaka 100 Tangu Kuanzishwa kwa Msikiti Mkuu wa Paris Yafanyika

Hawza/ Msikiti Mkuu wa Paris umefanya hafla ya kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, ambapo pia ulitoa heshima kwa askari Waislamu walioshiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, katika utambulisho wa historia ya msikiti huo imeelezwa kuwa; miaka mia moja iliyopita, jiji la Paris lilijenga Msikiti Mkuu wa Paris kwa heshima ya askari Waislamu kutoka makoloni ya Ufaransa waliopigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia.

Kwa sasa, msikiti huo ni sehemu muhimu ya eneo la Paris lenye shughuli nyingi, na wakati wa kuadhimisha miaka mia moja tangu kuanzishwa kwake, waumini wanaousalia wamekuwa wakitafakari maana ya kuwa Mwislamu nchini Ufaransa katika nyakati za sasa.

Mkurugenzi wa Msikiti Mkuu wa Paris, Bw. Hafiz, alisema kuwa; anaona msikiti huo kuwa ishara ya mazungumzo baina ya dini mbalimbali na utofauti wa imani nchini Ufaransa. Aidha, alieleza wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kidini nchini humo, hali ambayo amesema inahusishwa na migogoro ya Mashariki ya Kati pamoja na kampeni za uchaguzi zinazoendelea kuelekea uchaguzi wa rais wa mwaka ujao.

Aliendelea kusema kuwa; wakati msikiti huo ulipojengwa kwa mara ya kwanza, Rais wa Ufaransa wakati huo, Gaston Doumergue, alitangaza kwamba utofauti wa dini miongoni mwa Wafaransa ni fursa ambayo inaweza kuimarisha zaidi jamii ya taifa la Ufaransa. Bw. Hafiz alisema kuwa ujumbe huo ulikuwa mzuri na wenye thamani kubwa.

Bi. Fatima Chouchane, mmoja wa wanachama wenye shughuli nyingi katika Msikiti Mkuu wa Paris, alielezea masikitiko yake kuhusu vikwazo vinavyowekwa dhidi ya uvaaji wa hijabu kwa wanawake Waislamu katika shule za Ufaransa na baadhi ya maeneo ya kazi.

Alisema: "Naiomba Ufaransa iwaruhusu Waislamu waishi kwa mujibu wa imani yao na iwape uhuru wa kufanya uchaguzi wao wa kidini bila vikwazo."

Bi. Chouchane, kama ilivyokuwa kwa waumini wengine waliohudhuria hafla hiyo, alisisitiza ujumbe wa kuvumiliana, kuishi kwa maelewano na maridhiano katika maadhimisho ya miaka 100 ya Msikiti Mkuu wa Paris.

Chanzo: ABC News.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha